Shirika la Justdiggit lazindua app ya Kijani ili kuongeza kasi ya ukijanishaji kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika
Huu ni wakati wa Kijani! Leo hii, ikiwa ni siku ya Nanenane (sikukuu ya wakulima) nchini Tanzania, tunazindua app inayosubiriwa kwa hamu itakayotoa bure elimu ya ukijanishaji na itakayowanufaisha wakulima wadogowadogo milioni 350 walioko kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika. Tunaamini kuwa app ya Kijani inaweza kuongeza kasi ya kukijanisha sayari yetu, kwa hiyo, tunafurahi kusambaza mafanikio haya makubwa ulimwenguni kote!
Kijani ni nini?
Kijani ni aina mojawapo ya app ya kwenye simujanja, inayopatikana bure katika Google Play Store. App hii inawapa wakulima maarifa na ujuzi wote wanaohitaji ili waweze kukijanisha mashamba yao, hii ikiwa ni pamoja na masomo ya kidigiali yenye mbinu zilizothibitishwa ili kuongeza mavuno, kurutubisha ardhi na kuboresha maisha. Kijani inakusudia kuongeza matunda ya programu za ukijanishaji kwa kutumia ipasavyo simujanja kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.
“Mashirika mbalimbali hutoa elimu na kisha hutoweka, lakini app hii ni chaguo sahihi sana. Ninaweza kupakua app na inaendelea kubakia kwenye simu yangu. Sasahivi, ninanafasi nzuri zaidi ya kujifunza leo na kesho,” mkulima kutoka kijiji cha Owerendeke, mkoani Arusha, Tanzania.
Ushuari wa ukijanishaji mahususi kwa mtumiaji
App ya Kijani inatumia teknolojia ya taarifa ya GPS ili kutoa ushauri mahususi kwa mkulima mmojammoja kulingana na eneo alipo pamoja na mahitaji ya mtu. Hii inatuwezesha kuwasaidia wakulima kukijanisha ardhi zao kwa kiasi kikubwa bila sisi kulazimika kwenda katika maeneo yao.
Majaribio yaliyofanyika yanaonesha kwamba ushiriki wa wakulima kidigitali ni njia yenye ufanisi zaidi katika kuwafundisha mbinu za ukijanishaji. Baada ya kumaliza somo, washiriki wanaweza kufuatilia maendeleo yao na matokeo kwa kupakia picha za mashamba yao. Kisha, shirika la Justdiggit hutathmini matokeo ya jumla na kuhakiki matokeo yaliyowasilishwa kwa kutumia picha za satalaiti. Pia, wakulima wanaweza kusaidiwa kupitia dawati la usaidizi la mtandaoni na kutumiwa jumbe muhimu.
Kuharakisha uboreshaji wa mfumo wa ekolojia
Miezi kadhaa iliyopita, tumefanya majaribio ya kina na mamia ya wakulima wa Tanzania nchi nzima. Majaribio haya yameonesha kuwa mafunzo ya ana kwa ana si ya lazima tena; badala yake maudhui ya kidigitali pekeyake yanaweza kuleta matokeo mazuri. Hii inahamasisha imani yetu kuwa ukijanishaji kidigitali unaweza kuongeza kasi ya kukijanisha sayari yetu, hivyo kuchangia kuboresha mfumo wa ekolojia, kupunguza joto, na kuandaa jamii zinazoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
App ya Kijani inaweza kupakuliwa bure kabisa katika Google Play Store kuanzia tarehe 8 Agosti na inapatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu, app hii itapatikana katika nchi nyingine za Afrika na lugha mbalimbali zitaongezwa pia.
Maswali yanayoulizwa zaidi (MYZ)
Watu wengi wametuuliza maswali mazuri kuhusu Kijani. Ili kuweza kuyajibu yote, tumeandaa sehemu hii ya MYZ ili kukupa uelewa mzuri wa kile unachokitarajia kutoka kwenye app hii.
Je, watu wana simujanja? Na kama wanazo, intaneti wanayo?
Suala la mtandao na matumizi ya simujanja vinaongezeka kwa kasi barani Afrika. Ingawa inaweza kuchukua miaka kadhaa kwa wakulima wengi wadogowadogo kuwa na simujanja, faida za kulifikia kundi hili tayari zinatosha kuhalalisha utengenezaji wa app kwa ajili yao. Kwa uzoefu wetu, watu waliofundisha mbinu za ukijanishaji mara nyingi huwa wanakuwa mabalozi wa mbinu hizi. Pia, watumiaji wa app ya Kijani wanaweza kuwa mabalozi, kwa ambao bado hawana huduma ya intaneti.
Je, watu wanaweza kutumia app bila kuwasha intaneti?
App hii imetengenezwa kwa namna ambayo inaweza kutumika bila kutumia mtandao wa intaneti. Masomo mapya yanaweza kupakuliwa pekeyake mara tu baada ya kuwepo intaneti.
Je, wasiojua kusoma na kuandika wanaweza kutumia app hii?
Ndiyo, kwa sababu masomo yana video na sauti. Ingawa elimu kidogo inahitajika ili kuweza kupakua app na kuitumia, majaribio yetu yanathibitisha kuwa maudhui yanaweza kutumiwa hata na ambao hawajasoma.
Je, app hii itapelekwa nchi gani baada ya hapa?
Baada ya kuizidua nchini Tanzania, tutaipeleka nchini Kenya. Baada ya hapo, lugha mbalimbali zitaongezwa na tutaendelea kuisambaza ukanda mzima wa kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika. Pia, tutaifanya app iendane na mazingira kwa kuandaa masomo yanayohusu mazingira husika yenye picha zinazoendana na mazingira ya watu husika.
Je, kuna mambo gani katika app hii?
Kiini cha app ya Kijani ni sehemu ya maktaba ya masomo ambapo watu wanaweza kujifunza masomo yanayohusu namna ya kukijanisha ardhi zao, mfano Kisiki Hai. Sehemu hii inasaidiwa na sehemu ya wasifu ambapo mtumiaji anaweza kufuatilia maendeleo. Kuna sehemu ya taarifa ambapo hujumuisha taarifa na habari muhimu, na kuna sehemu ya msaada ambapo watu wanaweza kusaidiwa jinsi ya kutumia app na namna ya kutumia mbinu za ukijanishaji.
Je, taarifa binafsi za watumiaji zinalindwa?
Ndiyo, app ya Kijani inazingatia miongozo ya GDPR. Tunakusanya taarifa za mtumiaji zenye manufaa kwa mumiaji tu. Wakati wowote, mtumiaji anaweza kuondoa au kufuta taarifa zake.
Je, app hii inafadhiliwa na nani?
App hii itaendelea kuwa ya bure kwa kila mtu. App ya Kijani imeandaliwa na Justdiggit, shirika lisilo la kiserikali lenye makao makuu yake nchini Uholanzi. Utengenezaji wake umefadhiliwa na wadau mbalimbali kama vile National Postcode Lottery, Rabo Foundation, Milky Wire na Jingle Jam.