Kisiki Hai
ni nini?

Kisiki Hai ni njia ya kutunza maotea ya miti yanayochipua kutokana na Kisiki Hai au Mbegu za miti zilizodondoshwa ardhini na vinyesi vya wanyama au ndege.

Njia ya Kisiki Hai imeitwa ‘Mkombozi wa mazingira’ hasa katika maeneo kame, kwa sababu kuu nne:

1. Gharama nafuu,
2. Endelevu,
3. Rahisi kwa mtu yeyote,
4. Matokeo ya muda mfupi.

Elewa faida za Kisiki Hai na jinsi ya kutumia mbinu hii ya kukijanisha.

poster

Hatua 4 za kutunza
Kisiki Hai

Jifunze hatua nne za Kisiki Hai, ili uweze kuzitumia katika ardhi yako.

 • HATUA 1: Chagua
 • HATUA 2: Pogolea
 • HATUA 3: Alama
 • HATUA 4: Tunza

HATUA 1: Chagua

Chagua visiki hai ambavyo ungependa kuvitunza.

poster

HATUA 2: Pogolea

Chagua maotea machache yenye ubora zaidi kutoka kwenye kisiki na yakate maotea yaliyobaki.

poster

HATUA 3: Alama

Weka alama kwenye maotea uliyochagua kwa kufunga kitambaa chenye rangi inayoonekana ukiwa mbali.

poster

HATUA 4: Tunza

Tunza visiki vyako katika kipindi chote cha mwaka.

poster

CHAPOA TU!

Tunakupa kifupisho kwa ajili ya kumbukumbu rahisi: CHAPOA TU!

1. CHAgua: chagua visiki unavyotaka kutunza;

2. POgolea: chagua maotea machache yenye ubora Zaidi kutoka kwenye kisiki na yakate maotea yaliyobaki;

3. Alama: Weka alama kwenye maotea uliyochagua kwa kufunga kitambaa chenye rangi inayoonekana ukiwa mbali;

4. TUnza: Tunza visiki vyako katika kipindi chote cha mwaka!

Kumbukumbu rahisi: CHAPOA TU!

CHAPOA TU


Pamoja
turudishe uoto wa asili!

Wakulima wenzako wengi walianza kurudisha uoto wa asili, hivyo kuboresha ardhi yao. Hii inamaanisha wewe ni sehemu ya harakati kubwa ya kurudisha uoto wa asili! Hongera! Kwa Pamoja tunaweza kufanya Dodoma kuwa bustani ya Eden.

Jalome Sailowa mkulima kutoka Kijiji cha Mnyakongo mkoani Dodoma anasema:

“Tumekuwa tukikata miti kwa ajili ya kupata nafasi kwa ajili ya kilimo. Matokeo yake ni kumekuwa na upungufu wa uzalishaji na kuongezeka kwa mmomonyoko wa udongo. Kupitia LEAD Foundation na  Justdiggit tumekubaliana njia za kurudisha uoto wa asili kama Kisiki Hai ambazo zinarutubisha udongo, zinaboresha ulinzi wa mazao na maisha kwa ujumla.”

1_farmer spread the word_dig in_Justdiggit_farmer_Jalome Sailowa_Kisiki Hai_Mnyakongo_Dodoma_Tanzania

Maswali

Make-agreements

Swali la 1

Je tunawezaje kuzuia miti isiharibiwe na mifugo au moto?

Fanya makubaliano katika jamii. Uanzishwaji wa sheria ndogo ndogo na faini katika jamii kunaweza kusaidia kuzuia uchomaji wa misitu na kulisha mifugo hovyo.

Schermafbeelding 2021-04-13 om 14.16.59

Swali la 2

Je nitaweza kulima kwa kutumia trekta au ng’ombe kama nina miti shambani?

Ndiyo, unaweza! Acha miti shambani kwako kwa mitindo miwili:

 1. Kwenye mipaka inayozunguka shamba lako.
 2. Kwa kuacha miti kwa mistari katika shamba lako

Ukichagua njia ya pili, zingatia yafuatayo:

 • Acha nafasi ya kutosha kati ya mstari mmoja wa miti na mwingine, ili kuruhusu ng’ombe au trekta kupita kirahisi.
 • Mistari hii ua miti ianzie upande wa Mashariki, ili kuruhusu mwanga wa jua kumulika mimea yako;

Ushauri:

 • Acha miti angalau 20 katika kila ekari moja ya shamba lako.
 • Tenga eneo angalau la nusu ekari kwa ajili ya kustawisha miti tu ambayo itakusaidia kwa matumizi mbalimbali kama kuni, chakula cha mifugo pamoja na nguzo au mbao za kujengea nyumba.
3_inspire and mobilize farmers_communication_what we do_Justdiggit_farmer_Tanzania _ Kisiki Hai _ Mlanga _ may 2020 _ Hans Cosmas Ngoteya _ action pictures _ people

Swali la 3

Miti haita nyang’anyana maji, mwanga wa jua, au nafasi na mimea yangu?

Matokeo na vipimo  vya shamba yanaonyesha kuwa mavuno yanaongezeka baada ya kutumia njia ya Kisiki Hai!

 • Majani yanayo anguka kutoka kwenye miti yanatumika kama mbolea kwenye shamba.
 • Kivuli cha miti kinapunguza joto shambani.
 • Miti huleta mvua na unyevu.

Unaweza kuwasiliana na LEAD Foundation kama unahitaji msaada au kama unataka kujifunza zaidi kuhusu hii mada:

Anuani: Plot No. 125 Kilimani Box 1823 Dodoma

Simu: (+255) 026 2322786

Barua Pepe: info@leadfoundation.org

Tovuti: www.leadfoundation.org

Fanya juu chini filled with water

Fanya Juu na Fanya Chini

Kwa kutumia njia ya Fanya Juu na Fanya Chini, una chimba makingamaji katika shamba lako ili kuvuna maji ya mvua.

Fanya Chini ni Kingamaji ambalo linachimbwa upande wa juu wa shamba, udongo uliochimbwa unawekwa upande wa chini ili kutengeneza tuta ambalo litazuia maji kutoka mlimani kuingia shambani ili kuzuia mmomonyoko wa udongo wenye rutuba.

Fanya Juu ni kingamaji ambalo linachimbwa upande wa chini wa shamba, udongo uliochimbwa unawekwa upande wa juu wa shamba ili kutengeneza tuta ambalo litasaidia kubakiza maji ya mvua shambani na kuongeza upatikanaji wa maji kwa mimea. Mwishoni inasaidia kukijanisha ardhi yako!


KUHUSU

Shirika la LEAD Foundation lililopo mkoani Dodoma, Tanzania lina ujuzi na elimu ya kutosha katika utunzaji wa mazingira.

Shirika la Justdiggit linarudisha uoto wa asili katika mazingira yaliyoathirika barani Afrika, kwa kutumia mbinu kadhaa zakukijanisha, vyombo vya habari na teknolojia ya simu. Kwa pamoja tunarudisha uoto wa asili kwenye maeneo yaliyoharibika nchini Tanzania, hii inaleta athari chanya kwa mazingira na jamii. Lengo letu ni kuhamasisha mamilioni ya wakulima kuanza kurudisha uoto wa asili, kubadilisha maeneo makubwa ya ardhi kavu kuwa maeneo ya kijani kibichi na yenye rutuba.

Je, utajiunga nasi? Anza kurudisha uoto wa asili katika mazingira yako na ungana na Jaymondy katika mapinduzi ya kijani!

Maswali au maoni? Tafadhali wasiliana na LEAD Foundation:

Anuani: Plot No. 125 Kilimani Box 1823 Dodoma

Simu: (+255) 026 2322786

Barua Pepe: info@leadfoundation.org

Tovuti: www.leadfoundation.org

Redio kwa mkulima

Jifunze jinsi ya kukijanisha kwa kupitia redio

Kwa kushirikiana na Farm Radio International na Dodoma FM tumetengeneza vipindi vya redio kwa ajili ya mkulima, ambavyo vimerushwa katika mkoa mzima wa Dodoma.  Katik hivi vipindi unajifunza kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, faida za Kisiki Hai na jinsi ya kukitumia. Kipindi hiki kina mahojiano, igizo, vichekesho na maswali kutoka kwa wasikilizaji. Tunakutakia usikilizaji mwema.

Sikiliza vipindi 16 hapo chini!

Tunakutakia Usikilizaji mwema!

Kipindi 1 cha redio: Utangulizi wa kipindi cha Kisiki Hai Redioni
Kipindi 2 cha redio: Athari za mabadiliko ya tabia-nchi katika shamba lako
Kipindi 3 cha redio: Maana na historia ya Kisiki Hai
Kipindi 4 cha redio: Faida zitokanazo na Kisiki Hai
Kipindi 5 cha redio: Simulizi za mafanikio ya Kisiki Hai
Kipindi 6 cha redio: Chagua Visiki Hai
Kipindi 7 cha redio: Kupogolea Visiki Hai
Kipindi 8 cha redio: Kuweka alama na tunza
Kipindi 9 cha redio: Hofu ya kutekeleza njia ya Kisiki Hai
Kipindi 10 cha redio: Changamoto za kutekeleza Kisiki Hai
Kipindi 11 cha redio: Chagua Visiki Hai
Kipindi 12 cha redio: Kupogolea Visiki Hai
Kipindi 13 cha redio: Kuweka alama na kutunza
Kipindi 14 cha redio: Simulizi za mafanikio ya Kisiki Hai
Kipindi 15 cha redio: Uvunaji wa maji ya mvua
Kipindi 16 cha redio: Kuwa sehemu ya harakati kubwa
5_inspire and mobilize farmers_communication_what we do_Justdiggit_farm_radio_show_kisiki hai_tanzania_dodoma